*UTANGULIZI, JARIDA LA SHUJAA*
Kufika kilele cha maadhimisho ya siku ya sikoseli duniani, Taasisi isiyo ya kiserikali ya Sickle Cell Disease Patients Community of Tanzania iliona vyema uhitaji wa kuwepo na Jarida la Sikoseli kwani uwasilishi wa taarifa pekee hautoshi mahitaji ya walengwa, tuliona uhitaji wa kuwepo chombo ambacho kitakuwa ni jukwaa la kutoa elimu na uelewa juu ya sikoseli kwa lengo kuu la kuleta ufahamu zaidi wa sikoseli kwa wanajamii. Ndio, unaweza kuhoji kuwa kwanini jarida hili? ilhali kuna majarida mengi ya afya tayari, na tunaweza kukujibu, kuwa Jarida ili ni muhimu kwani, litakuwa ni chombo muhimu kwa wanajamii wa Sikoseli Tanzania kwa kuwapa nafasi ya kujenga hoja mbalimbali zinahusu ugonjwa wa sikoseli, pia litasaidia kuwa chanzo cha Taarifa za Ulimwengu wa sikoseli kwa walengwa, kikubwa zaidi Jarida ili litakuwa ni mwendelezo wa harakati za taasisi yetu katika kueneza elimu na uelewa wa ugonjwa wa Siko Seli.
Kama wahariri wakuu wa Jarida la Shujaa, lengo letu halikuwa elimu na uelewa tu bali pia kuupa kipaumbele ugonjwa wa sikoseli kwani tukiangalia takwimu zinaonyesha kuwa watoto 300,000 uzaliwa na Sikoseli Tanzania kila mwaka na pia katika watoto 1000 wanaozaliwa, mmoja anazaliwa na Sikoseli kila siku, kuongeza hapo kwa mujibu wa Takwimu 20% ya Watanzania wana vinasaba vya ugonjwa wa Siko Seli; Hivyo Jarida hili ni muhimu kwani litamulika ugonjwa wa Siko Seli na changamoto zote zinazohusika na Sikoseli.
Jarida la Shujaa ni kama ndege apazaye sauti katika majira kwa matumaini kuwa jamii itasikiliza na kuelewa kuhusu ugonjwa wa Siko Seli.
Hivyo, basi kama mdau tunachukua nafasi hii kuwaalika katika uzinduzi rasmi wa Jarida La Shujaa, Jarida la Kwanza la Sikoseli Tanzania.
Ni matumaini yetu kuwa utashirikiana nasi katika harakati hizi za maendeleo ya jamii katika kuhakikisha kuwa jamii inapata elimu na uelewa juu ya sikoseli.
Shukrani.